Luke 14

Isa Nyumbani Mwa Farisayo

1 aIkawa siku moja Isa alipokuwa amekwenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo siku ya Sabato, watu walikuwa wakimchunguza kwa bidii. 2Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili. 3 bIsa akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?” 4Wakakaa kimya. Hivyo Isa akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.

5 cKisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ng’ombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?” 6Nao hawakuwa na la kusema.

Unyenyekevu Na Ukarimu

7 dAlipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu: 8 e“Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe. 9Kama mkifanya hivyo yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa. 10 fBadala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule mwenyeji wako atakapokuona atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote. 11 gKwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”

12Kisha Isa akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. 13 hBali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, 14 inawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

Mfano Wa Karamu Kuu

(Mathayo 22:1-10)

15 jMmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Isa, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya Ufalme wa Mungu!”

16 kIsa akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi. 17 lWakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’

18“Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’

19“Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ng’ombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’ 20 mNaye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’

21 n“Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’

22“Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’

23“Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa. 24 oKwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”

Gharama Ya Kuwa Mwanafunzi

(Mathayo 10:37-38)

25Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukisafiri pamoja na Isa, naye akageuka, akawaambia, 26 p“Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. 27 qYeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

28 r“Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’

31“Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000? 32Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani. 33 sVivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Chumvi Isiyofaa

(Mathayo 5:13; Marko 9:50)

34 t“Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, itafanywaje ili iweze kukolea tena? 35 uHaifai ardhi wala kwa lundo la mbolea, bali hutupwa nje.

“Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
Copyright information for SwhKC